Wednesday, February 5, 2014


Stori: Waandishi Wetu
MPASUKO mkubwa umeikumba tasnia ya filamu Bongo baada ya baadhi ya wasanii wanaong’ara kuchukua kadi rasmi za kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Risasi Mchanganyiko linakupa zaidi.
Wasanii walojiunga CCM wakiwa katika picha ya pamoja na mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete.
Tukio hilo lilitokea juzi, Jumapili jijini Mbeya kulipokuwa na sherehe za maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa chama hicho ambapo mgeni rasmi alikuwa ni mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais Jakaya Kikwete.
Mashabiki mbalimbali wa sinema za Kibongo, waliingia kwenye mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii, mara baada ya wasanii hao kuonesha uamuzi wao, kila mmoja akieleza mtazamo wake.
WASANII WENYEWE
Baadhi ya wasanii waliochukua kadi za CCM ni pamoja na Jacob Steven ‘JB’, Single Mtambalike ‘Richie’, Irene Uwoya, Haji Salum ‘Mboto’, Tamrina Posh ‘Amanda’, Blandina Chagula ‘Johari’, Wastara Juma na Haji Adam ‘Baba Haji’.
MIJADALA
Watoa maoni walikuwa na mawazo tofauti kuhusiana na uamuzi wa wasanii hao wenye mashabiki wengi, wengine wakiwapongeza huku upande wa pili ukiwashutumu kwa maelezo kuwa wanawagawa mashabiki wao.
Mtoa maoni aliyejitaja kwa jina la Mussa Juma aliandika: “Sijui hawa wasanii wetu watakua lini? Huwezi kuonesha itikadi yako ya kisiasa wakati una mashabiki wengi. Hapo wamechemka. Mfano mimi siyo CCM na siwezi kununua tena filamu za JB.”
IPYANA LWIGA:
“Hii ndiyo demokrasia, unawavuta watu wajiunge kwako kwa kuwapa usafiri na mahitaji yote muhimu! Wameona mbali sana, nawapongeza sana! Wajifunze kwa Marlaw!”
BENATUS MARWA NYAMBORI:
“Huo ni uamuzi wao. Hauhusiani na kazi zao. Kama umechukia, chukua kazi zao zote piga moto. Kiukweli Chadema mnafikiri watu wengi wanawasapoti? Hapana... huko vijijini wanakuja kuangalia helikopta maana hawajawahi kuiona.”
JACOBS KING:
“Sasa hivi ndiyo watakoma kabisa, najua hakuna wa kununua kazi zao, wataibiwa mpaka wakome, CCM wanataka kuwatumia kwenye kampeni mikoani ili wawavutie wananchi kwenye mikutano yao lakini kwa sasa Watanzania tunajielewa.”
COCU BATENGA:
“Wasanii wana haki ya kuchagua chama chochote wakipendacho. Wakati wa kazi ni kazi, siasa ni siasa. Mbona Sugu (Joseph Mbilinyi – Mbunge wa Mbeya Mjini) yupo bungeni? Mbona Afande Sele (Seleman Msindi) ametangaza kujiunga Chadema, mbona hayasemwi? Hakuna mantiki hapa.”
JB BUNGENI
Hivi karibuni, JB alitangaza nia yake ya kugombea ubunge ingawa bado hajataja jimbo, kitendawili cha atagombea kwa tiketi ya chama gani, kimeshateguka baada ya kuchukua kadi ya CCM.
Hata hivyo, minong’ono inasema kwamba, JB huenda atagombea Jimbo la Kinondoni (kwa sababu ndiyo eneo analoishi) au Same (kwa sababu ni mzaliwa wa huko).

0 comments:

Post a Comment