Monday, February 10, 2014

MKUU wa Idara ya Hamasa na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapindunzi (UVCCM), Paul Makonda alitembelea chumba cha habari cha Global Publishers Janurai 24 mwaka huu na kuzungumza na wanahabari.
Paul Makonda.
Ni mengi aliyoyasema mbele ya wanahabari. Leo tunakuletea yale yaliyojiri siku hiyo.
Mara baada ya kukaribishwa na Mhariri wa Habari, Makala na Uratibu wa Global Publishers, Luqman Maloto katika jukwaa ambalo lipo ndani ya chumba cha habari, Makonda alianza kumponda Mwanasheria wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kutokana na maelezo yake aliyowahi kuyatoa kuhusiana na mgogoro unaofukuta ndani ya chama chao.
Makonda alisema mgogoro huo unaonesha udhaifu mkubwa wa uongozi katika Chadema.
“Tunaposema kuwa Chadema kuna udhaifu wa uongozi, watu sasa wanatuelewa. Kuna dhana ya kubaguana kitu ambacho ni hatari kwa taifa,” alisema Makonda.
Baadhi ya wafanyakazi wa Global wakimsikiliza Makonda.
Hata hivyo alihojiwa kisa cha kuchukua muda mwingi kuzungumzia Chadema lakini naye akajibu harakaharaka kuwa amelazimika kufafanua mzozo wa chama hicho kutokana na Lissu kudai kuwa mgogoro wao unachangiwa na chama chake.
“Sisi CCM hatuhusiki kabisa na mgogoro huo ndiyo maana nimelazimika kutoa ufafanuzi hapa kwenu, nikiamini kuwa Lissu alisimama hapa hapa niliposimama na kukishutumu chama chetu, lakini muuliza swali hakunielewa kwa nini nimefafanua hilo,” alisema.
MAKUNDI KATIKA VYAMA
Makonda alisema hata hivyo kuwa kuna tatizo la kitaifa la makundi na kufafanua kuwa kigezo cha makundi ya vyama vya kisiasa linaweza kuligawa  taifa na kusababisha machafuko mabaya nchini.
“Hakuna haja ya kupandikiza chuki zisizokuwa na maana wala tija kwa vijana wa taifa letu kwani lengo letu ni kujenga nchi inayozingatia utawala bora na maisha mazuri kwa wananchi,” alisema.
Makonda ambaye aliwahi kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, alisema katika maisha ya siasa hakuna kitu kibaya kama kupandikiza chuki ya makundi kwa vijana wa taifa kwani huzaa mgawanyiko ambao si rahisi kuufuta.
Alishauri tabia hiyo iachwe mara moja kwa sababu ni hatari kwa taifa.
Alipoulizwa lengo kuu la umoja wao kwa sasa katika nchi yetu, Makonda alifafanua kuwa wanataka kuona vijana wanajisimamia kimawazo na kifikra ili waweze kuamua ni kiongozi yupi anaweza kuwaongoza na kusimamia majukumu ya kijamii ipasavyo.
CHUKI NDANI YA VYAMA VYA SIASA
“Hakika chuki hizi za vyama vya siasa zinaelekea kubaya sana ambapo tusipokuwa makini taifa linaweza kugawanyika vibaya, nawaomba vijana tuwe makini sana na siasa za kupandikiza chuki na badala yake waweze kujisimamia na kutoa uamuzi sahihi wa nani anafaa kuwa kiongozi wao,” alisema Makonda.
Aliku-mbushwa kuwa zamani Tanu na baadaye Chama Cha Mapinduzi kilikuwa na kawaida ya kuwaandaa vijana ili waje kuwa viongozi katika chuo ambacho kilikuwa kikiitwa Chuo Cha Kivukoni.
Akaelezwa kuwa kupitia chuo hicho na UVCCM wamepatikana viongozi mbalimbali ambao sasa wanaendesha au waliendesha nchi kama vile Rais Jakaya Kikwete, Edward Lowassa, Seif Khatibu, William Lukuvi na kadhalika. Je, hivi sasa viongozi ndani ya chama chao hawaandaliwi kupitia umoja wao?
Alikumbushwa pia kuwa enzi hizo vijana walipandikizwa uzalendo kupitia Jeshi la Kujenga Taifa, JKT lakini sasa hilo halimo, akaulizwa kwamba haoni kuwa hilo ni tatizo hapa nchini?
Makonda alikiri kwamba mpango wa kupeleka vijana katika Chuo cha Kivukoni na Jeshi la Kujenga Taifa ulisaidia sana kupata viongozi bora na wazalendo.
Alisema chama chake kimeona hilo na sasa kina mpango wa kujenga chuo cha ‘kupika’ viongozi huko Ihema Iringa na kinatarajiwa kukamilika mipango ya kifedha itakapokamilishwa.
“Ni kweli Chuo cha Kivukoni kilisaidia sana kupata viongozi waadilifu. CCM ina mpango wa kujenga chuo chake huko mkoani Iringa. Viongozi wamegundua kuwa kufanya hivyo kunasaidia kujenga uzalendo na ndiyo maana JKT imerudishwa,” alisema Makonda.
Kuhusu makundi ya urais ndani ya CCM, Makonda alisema anaamini chama kina taratibu zake za kupata mgombea na akasisitiza kuwa kinachoonekana sasa ni magenge tu ya watu kupita huku na kule lakini anaamini wakati ukifika mgombea kwa tiketi ya chama chake atapatikana.

0 comments:

Post a Comment