Monday, February 10, 2014


Stori: Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa
SHETANI bado anajifanya haogopi, kila kukicha anasababisha. Safari hii amemjaribu mtumishi wa Mungu, Nabii Nicolas Suguye wa Kanisa la Huduma ya Neno la Upatanisho lililopo Kitunda-Kivule jijini Dar es Salaam ambapo yupo katika hali mbaya kufuatia kulishwa sumu na mtu asiyejulikana, Uwazi lina mkasa mzima.
Nabii Nicolas Suguye.
SIKU YA TUKIO
Taarifa zilizolifikia gazeti hili juzi kutoka kwa waumini wake zinadai kuwa tukio hilo lilijiri Februari 2, 2014 ambapo nabii huyo mwenye karama ya uponyaji alikuwa madhabahuni akihubiri neno lenye mamlaka na matendo ya miujiza lakini ghafla alijisikia maumivu ya tumbo, mwili kukosa nguvu na kichefuchefu.
ASHINDWA KUENDELEA NA HUDUMA
Kwa mujibu wa baadhi ya waumini hao, ilifika mahali mtumishi huyo wa Mungu alishindwa kuendelea na mahubiri, ikabidi atolewe na huduma yake kuchukuliwa na wasaidizi wake.
HALI YAZIDI KUWA MBAYA
“Baada ya kutolewa madhabahuni tuliamini hali itapoa baada ya kupumzika kidogo, lakini wapi? Hali yake ilizidi kuwa mbaya, sasa alikuwa hawezi kuzungumza sawasawa,” alisema muumini mmoja wa kanisa hilo.
AKIMBIZWA HOSPITALI YA AMI
Habari zaidi zinasema kuwa, ilipoonekana mtumishi huyo hapati nafuu, mkewe, Anna Suguye kwa ushirikiano na waumini wengine walichukua gari na kumkimbiza Hospitali ya African Medical Investment (AMI) iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam ambako alilazwa kwa matibabu ya awali. Ikumbukwe kuwa hata Askofu Moses Kulola alifia kwenye hospitali hiyohiyo.
WAUMINI WABUBUJIKWA MACHOZI
Wakati mchungaji huyo anapelekwa hospitalini, baadhi ya waumini walikuwa wakibubujikwa machozi kwa vile  walikuwa hawajui hatima ya kiongozi wao huyo.
UWAZI LATINGA KANISANI
Baada ya kuzinyaka taarifa hizo, Jumamosi iliyopita Uwazi lilitia timu kanisani kwa nabii huyo.
Ilikuwa vigumu kumpata kwani baadhi ya watumishi walidai hayuko katika afya ya kuonana na watu baada ya kutoka hospitalini.
Hata hivyo, muda mfupi baadaye mtumishi huyo wa Mungu aliwasili akiwa na mke wake. Alionekana amedhoofu pia hana raha.
ALIFUNGUKIA UWAZI
Baada ya salamu, Uwazi lilijitambulisha kwa mtumishi huyo na kumpa pole kwa yaliyomkuta ambapo alisema:
“Kwanza namshukuru Mungu wangu amenipigania hadi leo hii naongea nanyi. Kwa mujibu wa daktari nililishwa sumu kali sana japokuwa hakuniambia ni aina gani. Ila aliniahidi majibu kamili nitayapata baadaye leo.”
ILIKUWAJE?
“Nakumbuka ilikuwa Januari 28, mwaka huu ndipo nilianza kupata maumivu makali. Nilikuwa nikiendelea na ibada kanisani wiki nzima huku nikipata maumivu.
“Hata hivyo, nilikuwa nasali bila kujua ni kitu gani kilikuwa kikinisumbua kwenye mwili wangu. Nilifikiri ni ugonjwa wa kawaida ambao ningeweza kupata nafuu haraka lakini haikuwa hivyo.
KILICHOMKABILI
Nabii Suguye aliendelea kusema kuwa kikubwa kilichokuwa kikimsumbua kwa wakati huo ni kutapika huku mwili ukifa ganzi ndipo siku ya ibada akazidiwa na kukimbizwa hospitali.
“Pia daktari aligundua presha yangu ilishuka sana, nilitundikiwa dripu ya maji na kuchomwa sindano ya kupunguza maumivu.
“Hata hivyo haikusaidia, ikabidi wanichome sindano nyingine na kuchukua vipimo vya damu na picha ya X-ray, hawakubaini kitu. Halafu pia nikawa sipati choo, nikijisaidia inatoka damu.
SUMU YA MUDA MREFU
“Vipimo walivyochukua baadaye walibaini sumu niliyolishwa ilikuwa ya muda mrefu, tena ni Mungu bado ananipenda kwani sumu hiyo daktari alisema ni kali na nisingeweza kuchukua muda mrefu nikiwa hai,” alisema Suguye.
AWATUHUMU WABAYA WAKE
Akizungumzia hisia zake juu ya nani yuko nyuma ya sumu hiyo, Nabii Suguye alisema:
“Huenda wakawa wapinzani wangu wa huduma ya Mungu lakini kumjua ni nani, ilikuwa wapi na lini nilipewa si rahisi.”
HATAKI KUONANA NA MTU BAADA YA UWAZI
Suguye alisema baada ya mazungumzo na gazeti hili asingependa kuonana na mgeni mwingine yeyote kwa sababu bado hajapona sawasawa.
MAARUFU WALIOWAHI KULISHWA SUMU
Baadhi ya watu wenye majina makubwa waliowahi kulishwa sumu na kunusurika kifo ni Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima (hakutaja hospitali), msanii wa filamu za Bongo, Illuminata Poshi ‘Dotnata’ (alikimbizwa Lugalo) na aliyewahi kuwa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, SACP Charles Kenyela (alikimbizwa TMJ). Wote hawakukumbuka siku ya kukutwa na tukio.
UWAZI HADI HOSPTALI YA AMI
Juzi, Uwazi lilifika Hospitali ya Ami na kuulizia undani wa sumu aliyolishwa Nabii Suguye lakini daktari aliyekuwa zamu alisema hana kibali cha mtumishi huyo wa Mungu cha kutoa siri ya ugonjwa wake.
NABII ARUDIWA
Baada ya kutoka Ami, Uwazi lilimpigia nabii huyo na kumuuliza kama alishapata majibu ya daktari.
“Nilikwenda, wamesema naendelea vizuri. Walinipa dawa za aina mbili tofauti. Kuhusu sumu waliniambia ilibainika kwenye haja kubwa na ilikuwa kali sana,” alisema Suguye.


Stori: Na Igenga Mtatiro, Tarime
MDUNGUAJI wa watu takriban tisa wilaya ya Tarime mkoa wa mara, alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime baada ya kuzidiwa na vipigo vya Jeshi la Polisi, akigoma kutaja washirika wake.
Taarifa zilizotolewa na mganga mfawidhi wa Hospitali hiyo Roberty Onesmo zilisema muuaji huyo, Charles Range Kichune (38) alifariki dunia akiwa amelazwa katika wodi namba 8 Hospitalini hapo.
Onesmo alisema kuwa marehemu huyo ambaye mwili wake umehifadhi katika chumba cha kuhifadhia maiti, alifariki muda mfupi majira ya saa 10.00 usiku wa kuamkia juzi, baada ya kufikishwa na askari Polisi.
Mhalifu huyo ambaye ni mkaazi wa kitongoji cha Ronga kijiji cha Kenyamanyori kata ya Turwa wilaya ya Tarime, alikamatwa na askari Polisi mkoani Tanga alikotorokea baada ya kufanya mauaji ya watu tisa na kuwajeruhi wengine na kisha kuwapora vitu mabli mbali.
Jeshi la Polisi Tarime na Rorya na askari wa mkoa wa Tanga kwa ushirikiano walifanikiwa kumkamata siku ya Februali 6, mwaka huu jioni baada ya kukimbia wilayani hapa, alipojificha kwa muda kwa rafiki yake, mhalifu Marwa Keryoba wa mtaa wa Nyabisare manispaa ya Musoma.
Katika upekuzi nyumbani kwa rafiki yake ambaye aliuawa na askari polisi Februali 7 mwaka huu asubuhi katika mtaa huo, baada ya kukaidi amri na kuwarushia risasi, kulikutwa silaha ya aina ya SMG iliyokatwa kitako na mtutu ambayo Charles Range Kichune maarufu ‘’KENONKE’ alikiri kuitumia katika matukio ya mauaji na unyan’ganyi kwa wananchi 9.
Muuaji huyo alikiri kuifunga tochi silaha hiyo iliyotumika kumulika wakati wa kuendesha matukio hayo ambapo miongoni mwa watu waliouawa ni pamoja na mstaafu wa Jeshi la wananchi (Jwtz) na komando ambaye ni mtoto wa marehemu Meja Jenerali Mwita Marwa (Wabachira).
Kamanda wa Polisi Tarime na Rorya Justus Kamugisha alithibitisha kukamatwa kwa muuaji huyo mkoani Tanga, na silaha hiyo ya kivita pamoja na simu na vitu mbali mbali alivyovipora kwa watu waliouawa na kujeruhiwa katika vijiji vya Mogabiri, mjini Tarime, Nkende ,Rebu na Nyamwaga.
Aidha kamanda Kamugisha alithibitisha kufariki dunia muuaji huyo katika Hospitali hiyo baada ya kupelekwa kupatiwa matibabu na kwamba Jeshi la Polisi Tarime na Rorya linaendelea kuwasaka wahalifu wengine.


Mbunge wa Mbeya Mjini Chadema, Joseph Mbilinyi 'Sugu'.
Na Ojuku Abraham
UCHAGUZI mkuu wa Rais, wabunge na madiwani chini ya mfumo wa vyama vingi nchini, utafanyika kwa mara ya tano mwakani, huku kwa mara ya kwanza, chama tawala, CCM kikihofu kukutana na upinzani mkali, pengine kuliko wakati mwingine wowote.
Hofu hii, haitokani na kufanya kwake vibaya katika utekelezaji wa Ilani yake ya Uchaguzi iliyoipatia ushindi uchaguzi uliopita, bali kikubwa, ni kukubalika kwa vyama vya upinzani, hasa Chadema, ambacho kwa sasa ndicho kinaongoza Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni.
Kuelekea uchaguzi huo mkuu, safu hii ilifanya mahojiano na Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Simon Mbilinyi maarufu kama Sugu, ili pamoja na mambo mengine, kuelezea mtazamo wake juu ya tukio hilo kubwa kabisa kisiasa nchini.
Swali: Sisi tulio nje ya Chadema, tunafahamu kuna mgogoro mkubwa ndani ya chama chenu, wewe uko ndani, unaweza kutueleza kwa kifupi kilichopo?
Sugu: Hakuna mgogoro wowote ndani ya Chadema, kilichopo ni kwamba mwanachama mmoja na kiongozi alikiuka maadili, vikao vikamjadili na uamuzi ukachukuliwa. Chadema inajiandaa kuchukua nchi, lazima tuonyeshe kwa vitendo kwamba tukiwa pale, maadili ni kitu muhimu kabisa, lazima tutoe kibanzi ili kuwa tayari kuiona boriti.
Sisi siyo kama CCM, wanaogopana, hawawezi kuchukua hatua. Tumefika hadi vijijini ambako wanasema hatufiki, umati wa watu wanaokuja kutusikiliza unaonyesha wazi hakuna mgogoro, ni uamuzi tu ambao hata hivyo mjadala wake ulishafungwa.
Swali: Unamzungumziaje Zitto Kabwe, nadhani alikuwa mmoja wa vijana walioku-impress kuingia katika siasa.
Sugu: No, Zitto siyo, mimi nilikuwa impressed zaidi na Mnyika (John).
Swali: Jeuri ya Chadema kuamini kwamba itachukua nchi mwakani inatokana na nini?
Sugu: Siyo jeuri, bali ni hali halisi. Kwanza CCM imeishiwa mbinu na taifa liko tayari kwa mabadiliko.
Kinana (Abdulrahman, Katibu Mkuu, CCM) na Nape (Nnauye, Katibu wa Itikadi, CCM) wanaenda kwa wananchi wanawasaidia kupalilia mazao yao (kicheko), hii ni dhahiri kwamba hawajui mahitaji yao, wakulima hawahitaji kusaidiwa kupalilia, wao walitakiwa kuwaeleza CCM ina mpango gani kuhakikisha mbolea inawafikia kwa wakati na bei muafaka, wasichokijua ni kwamba wanapokwenda kwa staili ile wanawaongezea hasira.
Jambo jingine ni kuwa taifa lipo tayari kwa mabadiliko. Kote tunakopita, wananchi wanaonekana kabisa kuhitaji mabadiliko, tunafika hadi katika maeneo ambayo hata gari halijawahi kufika, wanapotuona sisi tumekwenda na helikopta, wanasema kama nyinyi mmeweza kuleta ndege, basi hata uwanja wake tutapata.
Nchi imeiva mzee, ni muda tu, ukichanganya na haya mambo ya CCM kuogopana kuchukuliana hatua, ukichukulia na muda uliobaki, njia ni nyeupe kwa Chadema kuichukua nchi.
Angalia, sisi tupo 49 tu bungeni, lakini tunatoa hoja ambazo zinakubalika na kufanyiwa kazi, zile zinazokataliwa, tunawapelekea wananchi na wao wanatuelewa, ndiyo maana mara nyingi tumetoka bungeni na kuwafuata wananchi kuwaeleza ndipo serikali inakubali. Wewe mwenyewe ni shuhuda wa jinsi serikali ilivyobadili mambo mengi baada ya sisi kutoka bungeni na kuwashtakia kwa wananchi.
Swali: Ni ugumu gani unafikiri utawakabili mkijiandaa kuichukua nchi?
Sugu:  Hakuna ugumu, CCM imekwisha, ukiangalia mpasuko wao na muda uliobaki, hakuna ugumu kabisa. Kitu cha msingi ni uboreshwaji tu wa daftari la wapiga kura, vijana wajiandikishe kwa wingi, ingawa siwadharau pia akina mama kwa sababu pale Mbeya ni mtaji wangu mkubwa sana.
Swali: Ukiwa Mbunge, unadhani malengo yako yametimia kwa asilimia ngapi?
Sugu: Ni zaidi ya asilimia 90 na mengine yamezidi 100. Nilichoahidi kukifanya mimi kama mimi nimefanikiwa kwa asilimia 90, mengine niliahidi kusimamia na kufuatilia, haya yamezidi sana. Nape alikuja Mbeya anawaambia watu kuwa eti lile jimbo ni la CCM, na mimi ni mpangaji tu.
Nataka nimwambie kuwa mimi ni kama Mpemba au Mkinga, nimekuja Kariakoo nikakuta jengo chakavu, nikalipiga chini (kubomoa) na kujenga ghorofa, ninao uwezo wa kuwapangisha niliowakuta na ndicho kilichopo Mbeya.
Swali: Utagombea tena Ubunge mwakani?
Sugu: Yaaa, nitagombea, lakini sisi hatuzungumzii sana ubunge, tunazungumzia Halmashauri, tunataka kuchukua halmashauri, pale ndiyo kila kitu.
Swali: Unauzungumziaje msimamo wa Chadema wa serikali tatu katika Katiba mpya tunayoelekea kuipata?
Sugu: Tunataka watu waelewe kuwa Chadema haina msimamo katika hili, sisi tunafuata matakwa ya wananchi, wananchi wametaka serikali tatu na Warioba (Joseph, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba) ambaye ni CCM, aliwasilisha maoni ya wananchi, alisema asilimia 61 wametaka serikali tatu, sasa kwa nini useme msimamo wa Chadema, tunataka matakwa ya wananchi yazingatiwe kwa sababu hiyo ni katiba yao.

MKUU wa Idara ya Hamasa na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapindunzi (UVCCM), Paul Makonda alitembelea chumba cha habari cha Global Publishers Janurai 24 mwaka huu na kuzungumza na wanahabari.
Paul Makonda.
Ni mengi aliyoyasema mbele ya wanahabari. Leo tunakuletea yale yaliyojiri siku hiyo.
Mara baada ya kukaribishwa na Mhariri wa Habari, Makala na Uratibu wa Global Publishers, Luqman Maloto katika jukwaa ambalo lipo ndani ya chumba cha habari, Makonda alianza kumponda Mwanasheria wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kutokana na maelezo yake aliyowahi kuyatoa kuhusiana na mgogoro unaofukuta ndani ya chama chao.
Makonda alisema mgogoro huo unaonesha udhaifu mkubwa wa uongozi katika Chadema.
“Tunaposema kuwa Chadema kuna udhaifu wa uongozi, watu sasa wanatuelewa. Kuna dhana ya kubaguana kitu ambacho ni hatari kwa taifa,” alisema Makonda.
Baadhi ya wafanyakazi wa Global wakimsikiliza Makonda.
Hata hivyo alihojiwa kisa cha kuchukua muda mwingi kuzungumzia Chadema lakini naye akajibu harakaharaka kuwa amelazimika kufafanua mzozo wa chama hicho kutokana na Lissu kudai kuwa mgogoro wao unachangiwa na chama chake.
“Sisi CCM hatuhusiki kabisa na mgogoro huo ndiyo maana nimelazimika kutoa ufafanuzi hapa kwenu, nikiamini kuwa Lissu alisimama hapa hapa niliposimama na kukishutumu chama chetu, lakini muuliza swali hakunielewa kwa nini nimefafanua hilo,” alisema.
MAKUNDI KATIKA VYAMA
Makonda alisema hata hivyo kuwa kuna tatizo la kitaifa la makundi na kufafanua kuwa kigezo cha makundi ya vyama vya kisiasa linaweza kuligawa  taifa na kusababisha machafuko mabaya nchini.
“Hakuna haja ya kupandikiza chuki zisizokuwa na maana wala tija kwa vijana wa taifa letu kwani lengo letu ni kujenga nchi inayozingatia utawala bora na maisha mazuri kwa wananchi,” alisema.
Makonda ambaye aliwahi kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, alisema katika maisha ya siasa hakuna kitu kibaya kama kupandikiza chuki ya makundi kwa vijana wa taifa kwani huzaa mgawanyiko ambao si rahisi kuufuta.
Alishauri tabia hiyo iachwe mara moja kwa sababu ni hatari kwa taifa.
Alipoulizwa lengo kuu la umoja wao kwa sasa katika nchi yetu, Makonda alifafanua kuwa wanataka kuona vijana wanajisimamia kimawazo na kifikra ili waweze kuamua ni kiongozi yupi anaweza kuwaongoza na kusimamia majukumu ya kijamii ipasavyo.
CHUKI NDANI YA VYAMA VYA SIASA
“Hakika chuki hizi za vyama vya siasa zinaelekea kubaya sana ambapo tusipokuwa makini taifa linaweza kugawanyika vibaya, nawaomba vijana tuwe makini sana na siasa za kupandikiza chuki na badala yake waweze kujisimamia na kutoa uamuzi sahihi wa nani anafaa kuwa kiongozi wao,” alisema Makonda.
Aliku-mbushwa kuwa zamani Tanu na baadaye Chama Cha Mapinduzi kilikuwa na kawaida ya kuwaandaa vijana ili waje kuwa viongozi katika chuo ambacho kilikuwa kikiitwa Chuo Cha Kivukoni.
Akaelezwa kuwa kupitia chuo hicho na UVCCM wamepatikana viongozi mbalimbali ambao sasa wanaendesha au waliendesha nchi kama vile Rais Jakaya Kikwete, Edward Lowassa, Seif Khatibu, William Lukuvi na kadhalika. Je, hivi sasa viongozi ndani ya chama chao hawaandaliwi kupitia umoja wao?
Alikumbushwa pia kuwa enzi hizo vijana walipandikizwa uzalendo kupitia Jeshi la Kujenga Taifa, JKT lakini sasa hilo halimo, akaulizwa kwamba haoni kuwa hilo ni tatizo hapa nchini?
Makonda alikiri kwamba mpango wa kupeleka vijana katika Chuo cha Kivukoni na Jeshi la Kujenga Taifa ulisaidia sana kupata viongozi bora na wazalendo.
Alisema chama chake kimeona hilo na sasa kina mpango wa kujenga chuo cha ‘kupika’ viongozi huko Ihema Iringa na kinatarajiwa kukamilika mipango ya kifedha itakapokamilishwa.
“Ni kweli Chuo cha Kivukoni kilisaidia sana kupata viongozi waadilifu. CCM ina mpango wa kujenga chuo chake huko mkoani Iringa. Viongozi wamegundua kuwa kufanya hivyo kunasaidia kujenga uzalendo na ndiyo maana JKT imerudishwa,” alisema Makonda.
Kuhusu makundi ya urais ndani ya CCM, Makonda alisema anaamini chama kina taratibu zake za kupata mgombea na akasisitiza kuwa kinachoonekana sasa ni magenge tu ya watu kupita huku na kule lakini anaamini wakati ukifika mgombea kwa tiketi ya chama chake atapatikana.


Stori: Richard Bukos na Makongoro Oging
MTOTO Grace Simon (14) aliyewahi kuripotiwa na gazeti hili kuwa anapata mateso kutokana na mwili wake kuzidi kufumuka kila kukicha, hatimaye amefikishwa Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.
Akizungumza kwa masikitiko mama wa mtoto huyo, Ashura Ally alisema baada ya kuhangaika sehemu mbalimbali zikiwemo hospitali za Wachina, kwenye huduma za maombezi na sehemu nyinginezo bila mafanikio, sasa mwanaye huyo amefikishwa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
“Awali mwanangu alifanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa na tatizo kwenye ini na homoni zimepoteza uwiano na kumfanya afumuke bila mpangilio,” alisema mama huyo.
Mama wa mtoto ameendelea kuomba msaada wa hali na mali ikiwemo ushauri unaoweza kuokoa afya ya mwanaye kupitia namba 0769319446 na 0719465443.


Jokate Mwegelo.
Stori: Hamida Hassan na Gladness Mallya
THE big boss wa Kidoti, Jokate Mwegelo ambaye pia ni staa wa sinema na Bongo Fleva, amefichua siri ya kupatana na Wema Isaac Sepetu akisema kuwa sababu ya yeye kuonekana kwenye jukwaa moja na aliyekuwa hasimu wake huyo ni kutafuta amani ya moyo aliyokuwa ameikosa si kweli kwamba alisukumwa na nguvu ya pombe.
Jokate akicheza sambamba na Wema ndani ya Ukumbi wa Triple A, Arusha.
Wawili hao walipatana hivi karibuni wakiwa jijini Arusha.
Akizungumza na gazeti namba moja la burudani Bongo, Ijumaa Wikienda, Jokate alisema ilipokaribia siku ya kwenda Arusha, Wema alimkaribisha kwenye shoo yake iliyofanyika jijini humo lakini alimwambia kuwa amebanwa ila akamuahidi kwamba akimaliza mambo yake atakwenda kumsapoti.
“Wema aliondoka bila kujua kama nitakwenda lakini nilipopanga ratiba yangu ikakaa sawa, niliamua kwenda na kumfanyia ‘sapraizi’ na si kweli kwamba nilisukumwa na nguvu ya pombe,” alisema Jokate.
Jokate alisema kwamba hakushauriwa wala kujadiliana na mtu yeyote isipokuwa aliamua mwenyewe kufanya jambo hilo ambalo lilikuwa likimkosesha faraja kwa muda mrefu.
“Nimeamua kumaliza mabifu kwa sababu nilikosa amani ninayoitaka kwa muda mrefu. Ukweli Wema alinikaribisha, nikaona ndiyo sehemu ya kutimiza lengo langu la kupatana naye,” alisema Jokate ambaye aliingia kwenye gogoro na Wema baada ya kutembea na mpenzi wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.


Stori: Imelda Mtema
MAMBO hadharani! Penzi ‘hoti’ la mastaa mahiri wa filamu za Kibongo, Chuchu Hans na Vincent Kigosi ‘Ray’ kwa sasa limekuwa kama la njiwa kwani mara nyingi kila sehemu wapo pamoja na hakuna kificho tena.
Ray na Chuchu wakijiachia.
Chanzo chetu makini kilieleza kuwa mastaa hao wamekuwa wakionekana pamoja mara nyingi na hivi sasa inadaiwa kuwa wanaishi pamoja huku wakiwa na mtoto wa Chuchu aitwaye Danzel.
Mpashaji wetu huyo alizidi kudai kuwa kutokana na mapenzi hayo kukolea siku hadi siku, juzikati baadhi ya ndugu wa mastaa hao walianza vikao vya chini kwa chini ili kuhakikisha mwaka huu wasanii hao wanafunga ndoa lakini haijajulikana kama watafungia kanisani au msikitini kwa kuwa wana dini tofauti.
“Yaani sasa hivi hakuna siri hata chembe, ni fulu kujiachia. Mara nyingi wapo pamoja kila sehemu yaani kama njiwa,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kilizidi kudai kwamba mara nyingi Ray na Chuchu wanapenda kwenda kuogelea na kujiachia kama mke na mume kwenye hoteli moja maarufu (jina linahifadhiwa) iliyoko maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar huku wakijifotoa picha za kumbukumbu.
Baada ya kujazwa ‘info’ hizo na kumwagiwa picha za mastaa hao, gazeti hili lilimtafuta Chuchu kisha kumuuliza kuhusiana na penzi lake na Ray kuwa ‘shatashata’ ambapo alifunguka kuwa kama kuna mtu anawaona wakiwa pamoja ni kwa sababu hivi sasa eti wanaandaa ‘sinema’ yao wawili.
Alipotafutwa Ray ili kuulizwa kuhusiana na ishu hiyo, simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa kwa muda wa nusu saa.