Friday, February 7, 2014


ZUWENA Mohamed, ni mdada anayefanya vizuri katika muziki wa mduara, ingawa pia anajulikana katika jamii ya watu wa filamu, ambako ni maarufu sana kwa jina la Shilole.
Shilole ana nyimbo kadhaa zinazomfanya kuwa mmoja kati ya wasanii wa mduara wanaopata shoo nyingi kwa sasa, huku kibao chake cha Nakomaa na Jiji kikiwa katika nafasi ya kwanza kati ya zinazofanya vizuri. Anazo nyimbo zingine pia, kama Paka la Baa, Dudu aliomshirikisha Q Chillar, Viuno tucheze, aliowashirikisha Kitokololo na Rich Mavoko, Lawama na nyinginezo.
Niwe mkweli, sijawahi kuvutiwa na jinsi anavyoufanyia kazi ubunifu wake maridhawa. Aina za nguo na uchezaji unamuondolea alama nyingi katika ufaulu. Ni msanii anayepaswa kubadili staili zake za kazi ili aweze kubeba mashabiki wa rika na akili zote, vinginevyo kuna kitu watakosa, hata kama wanapata shoo nyingi!
Mara kadhaa siku za nyuma, Shilole aliwahi kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari, akisema ni ndoto yake kupata mwanaume wa Kizungu, kwani kwake yeye, waswahili ‘wanazingua’.
Katika kitu kilichoonekana kama kutimia kwa ndoto yake, wiki moja na ushee iliyopita, gazeti dada na hili, Amani, lilitoa picha na habari ikimuonyesha msichana huyo akiwa amepiga na mwanaume mmoja Kizungu, raia wa Uingereza, ambaye tulibahatika kupata jina lake moja tu, Ankar.
Katika habari hiyo, Shilole alimshukuru Mungu kwa kumtimizia ndoto zake. Kwamba aliyekuwa akimtafuta, hatimaye amemtia mikononi. Dada alisema alimpata mwanaume huyo katika moja ya shoo zake alizoalikwa huko majuu.
Nadhani ni mavuno ya ile cheza yake. Lakini siku chache baadaye, zikapatikana habari, ambazo uzuri alizithibitisha pia Shilole mwenyewe, kuwa mwanaume yule, ‘shemeji’ yetu Ankar, eti kumbe si riziki!
Maana ya mkasa huu ni kwamba Shilole alikurupuka, shida yake ilikuwa ni kupata bwana Mzungu, awe shoga, jambazi, mla watu au gaidi, kwake si hoja, anachohitaji ni Mzungu.
Angekuwa na weledi kidogo wa kutosha, suala la aina ya mume anayemtaka, hasa unapozungumzia uraia tofauti na wake, lilipaswa kufanywa kimyakimya. Na hata baada ya kumpata Ankar, alitakiwa kuwa na muda wa kutosha pia kumchunguza kabla hajaamua kutuweka wazi kuhusu shemeji yetu.
Angefanya hivi, angetambua mapema kuwa kumbe jamaa siyo, angemtosa na hakuna mtu angejua.
Lakini kutokana na haraka zake, na akiamini kabisa kuwa ni jambo la sifa kwake kuwa na bwana Mzungu, amejikuta akiumbuka, kwa sababu shemeji aliyetuletea ni kama Anti Bilali wa Uingereza!
Na hili siyo tatizo la Shilole peke yake, ulimbukeni huu wanao wadada wengi wa Kibongo, kuanzia mabeki tatu hadi mastaa wetu uchwara. Kwao, Wazungu ni kila kitu. Wakiwaona tu, ni kama Mbwa wanavyokosa ujasiri mbele ya Chatu, hujipeleka wenyewe, tena wakijisikia fahari kabisa.
Sisi wengine wenye misele ya hapa na pale, tunajua kuna Wazungu wengi tu choka mbaya na wakati mwingine wamekuwa wakitumiwa na waswahili wenzetu kurahisisha mambo hata kwa maofisa wa serikali, kwani nao wana ulimbukeni wa kupapatikia Wazungu bila hata kuwafahamu vizuri.
Ndiyo maana tuna kesi nyingi za dada zetu kulazimishwa kufanya mapenzi na mbwa, kwa sababu ya kupapatikia ngozi nyeupe. Labda Shilole awe angalau mfano wa kuweza kujifunza, siyo kila king’aacho ni dhahabu.
Kuna ndugu na jamaa zetu wapo kule China, wanatuambia kuna soko kubwa la machangudoa. Miongoni mwao, ukiachilia mbali hawa dada zetu wauza sura katika televisheni ambao kila siku huenda huko, pia kuna watu weupe kibao kutoka Ulaya Mashariki wanajiuza. Hawa ni Wazungu maskini tu, ambao akina Shilole wakiwaona wanajihisi ujiko kuturingishia.
Tunaambiwa, mtu akionekana na changudoa Mzungu, anadharaulika, kwa sababu wako ‘so cheap’. Na hata sisi akina kaka, tuacheni matambo na mademu wa Kizungu, ile ni rangi tu, lakini ukweli ni kwamba Wazungu halisi ni watu wanaodharau sana ngozi yetu.

0 comments:

Post a Comment