Saturday, February 8, 2014


JOTO la Bunge la Katiba, limeendelea kupanda ambapo jana Waziri wa Katiba na Sheria wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Abubakar Khamis Bakary, alijikuta akipingwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Alli Iddi, kuhusu msimamo wa Zanzibar katika Bunge hilo.
Abubakar alitaka wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka Zanzibar, waweke msimamo mmoja kabla ya kuingia katika Bunge hilo, ili watetee maslahi yao. Kwa mujibu wa Waziri huyo, lengo ni kuhakikisha kunafanyika marekebisho katika Muungano, ambayo kwa muda mrefu alidai yamekuwa kero.
Kabla ya Waziri huyo kuunga mkono hoja hiyo, baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, walitaka Serikali iweke mwongozo na msimamo kwa wajumbe wa Zanzibar watakaoshiriki katika Bunge la Katiba ili kuwa kitu kimoja na kuepuka kugawanyika.
Hata hivyo Balozi Seif alipinga hoja hiyo na kusema SMZ haina msimamo utakaoongoza wajumbe wa Bunge la Katiba wakati wa kujadili rasimu ya pili ya Katiba mpya.
Akiahirisha kikao cha Baraza la Wawakilishi hadi Mei 14 mwaka huu, Balozi Seif alisema fursa imetolewa kwa wajumbe watakaohudhuria Bunge la Katiba kujadili kwa kina na uhuru unaozingatia demokrasia.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina msimamo wala haijatoa mwongozo kuhusu Bunge la Katiba...wajumbe wenyewe ndiyo watakaofanya uamuzi wenye maslahi kwa Taifa,” alisema.
Alitaka wajumbe wa Bunge la Katiba, ambao ni wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wajumbe wengine 201 watakaotangazwa leo na Rais Kikwete, kuzingatia uzalendo, maslahi ya Taifa na mshikamano wa Watanzania. Alisema kila mshiriki wa Bunge la Katiba anapaswa awe huru katika mjadala ili kufanya uamuzi sahihi.
“Serikali inasisitiza tena kwamba haina msimamo kwa wajumbe wake watakaoshiriki Bunge la
Katiba...wabunge watakaochaguliwa wafanye uamuzi sahihi kwa maslahi ya Taifa,” alisema.
Naye Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu, aliwataka wajumbe wa Bunge la Katiba kujua mipaka ya kazi yao katika maandalizi ya Katiba na wahakikishe wanaboresha Katiba kwa niaba ya Watanzania na si kwa matakwa yao.
Akizungumza katika warsha iliyoandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la TADIP jana jijini Dar es Saam, Profesa Baregu alisema katika mambo yanayopaswa kurekebishwa ni pamoja na maneno yanayosomeka katika Katiba kwamba ‘mambo mengine’.
Alifafanua kwamba alisema neno hilo lina upana usio na ukomo hivyo ni vema hayo ‘mambo mengine’ yakafafanuliwa yaeleweke ni mambo gani.
Alisema kuna mambo mengi ya kujadili lakini kikubwa kinachojadiliwa hivi sasa ni muundo wa serikali ziwe ngapi na Muungano.
Profesa Baregu alisema kuna mambo mengi ya kujadili mbali na hayo akitolea mfano katika rasimu ya pili ya Katiba ibara ya 48 inahusu haki za wazee ambazo katika maelezo inafafanua fursa za wazee jambo ambalo linachanganya.
"Ibara hii inasema haki za wazee lakini kwanza haisemi mzee ni kuanzia miaka mingapi au mtu akiwa na mvi tu anatambulika kama mzee, pili ndani wanataja fursa za wazee, hii inachanganya fursa sio haki," alisema Profesa Baregu.
Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Hebron Mwakagenda akitoa mada katika mkutano huo alisema mambo ambayo jukwaa linatarajia kuyafanya ni pamoja na kuandaa mkutano wa watu 1,000 ambao utahusisha wabunge wote kujadili mambo ya Katiba na hasa Muungano na mgeni rasmi katika mkutano huo ni Rais Jakaya Kikwete.
Alisema wanataka kuendesha kura ya maoni kuwahoji Watanzania wanataka Serikali ngapi, ili kupata maoni yao.
"Mbali na hilo tunataka kukutana na wajumbe hao 201 wa Bunge la Katiba kuwapiga msasa wajielewe wajibu wao ndani ya Bunge na kwamba wakiwa bungeni wote ni sawa," alisema Mwakagenda.
Dk Ayoub Rioba, Mhadhiri Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema itakuwa jambo la aibu kama Bunge litaingiza mambo yao kwa siri.
Imeandikwa na Khatib Suleiman, Zanzibar na Regina Kumba, Dar
CHANZO HABARI LEO

0 comments:

Post a Comment